Tembo na Kiboko
Terkule Aorabee
Awwalu Sakiwa

Kuliishi mapacha wawili wa kiume, Tembo na Kiboko.

Siku moja, Hatima iliwapatia nafasi ya kufanya uchaguzi kati ya vitu viwili. "Chagua upofu au ukoma," Hatima iliwaamrisha.

Kiboko alitaka kuwa mwerevu. Kwa haraka, alichagua ukoma ili aweze kuendelea kuona. Tembo alichagua upofu.

1

Kiboko alikuwa mvulana mwenye hasira kwa sababu ya ukoma. Upofu ulimpatia Tembo uvumilivu. Tembo alihitaji usaidizi, lakini Kiboko alimtendea ukatili.

Halafu Tembo akapata Fimbo ya miujiza iliyomwezesha kutembea. Walinong'onezeana siri. Fimbo ilimsaidia Tembo kuwapiga maadaui.

2

Kwa sababu Kiboko alivipoteza vidole vyake, yeye pia alihitaji usaidizi. Tembo alimtendea wema.

Chakula kilipobaguliwa, Kiboko alimhitaji Tembo kukikata vipande na kukiweka kwenye viganja vyake. Kiboko hakufurahi.

3

Asubuhi moja, mama yao aliwabagulia viazi vikuu. Kwa sababu walikuwa na njaa, wavulana hao hawakusubiri viazi hivyo vipoe.

Kiboko aliviweka viganja vyake pamoja vikawa kama sahani. Akasema, "Niwekee sehemu yangu hapa."

4

Viazi vikuu vilikuwa moto sana hata vikachoma viganja vyao. Kiboko aliienua mikono yake juu na chini, kuvipoesha. Kiazi kilianguka mchangani.

Tembo aligeuzageuza kiazi chake kutoka mkono mmoja hadi mwingine bila kiazi kuanguka. Kiboko alikasirika.

5

"Tafadhali, nichukulie kiazi changu," Kiboko alimwuliza Tembo.

"Unajua kuwa sikioni," Tembo alimjibu. "Nipe mkono wako nikuonyeshe," Kiboko alisema.

Tembo alikipata kiazi, akakifuta mchanga kisha akampatia Kiboko.

6

Jioni, mama yao aliwatayarishia viazi vikuu pamoja na vipande vinne vya nyama. Tembo aliigusa ile nyama kwa kidole chake akahakikisha kuwa vilikuwa vipande vinne.

Kiboko hakumwona Tembo akivihesabu vile vipande vya nyama.

7

Kiboko alijaribu kuiba kipande kimoja cha nyama lakini akakiangusha. Wakati wa kugawa nyama ulipofika, Tembo aliuliza, "Si vipande vya nyama vilikuwa vinne?"

"Vilikuwa vitatu," Kiboko alidanganya. "Vilikuwa vinne," Tembo alisisitiza. "Kweli wewe ni kipofu?" Kiboko aliuliza.

8

Siku moja, walihisi njaa lakini mama yao alikuwa mbali. "Twende tucheze ili tuisahau njaa," Kiboko alipendekeza.

Tembo alikubali, kisha Kiboko akasema, "Twende tukaogelee mtoni." Alijua kwamba Tembo hakujua kuogelea. Alipanga kumuua nduguye!

Tembo aliongozwa na Fimbo akamfuata Kiboko.

9

Walipokuwa njiani, Kiboko aliingia kichakani. Alilichukua jiwe nzito na kuliweka kwapani huku akikoroma. Alikuwa bado anakoroma walipokuwa wanakwenda mtoni.

"Mbona anakoroma hivyo?" Tembo aliiuliza Fimbo.

10

Walipofika mtoni, Kiboko alisema, "Nitatangulia kuruka majini kisha nikusaidie kuogelea."

Alisonga mbali na Tembo akaliinua lile jiwe nzito na kulitumbukiza majini.

"Sauti hiyo ni ndogo sana kulingana na ukubwa wa Kiboko," Fimbo ilimnong'onezea Tembo sikioni.

11

Tembo aliiuliza Fimbo kuchunguza zaidi. Aliizungusha Fimbo kila mahali hata Fimbo ikamgonga Kiboko kwa nguvu. "Ayii!" Kiboko akalia na kuruka majini.

Fimbo ya miujiza ilimgeuza Kiboko akawa mnyama wa majini. Ilimgeuza naye Tembo akawa mnyama wa nchi kavu akiwa na mkonga.

12
You are free to download, copy, translate or adapt this story and use the illustrations as long as you attribute in the following way:
Tembo na Kiboko
Author - Terkule Aorabee
Translation - Ursula Nafula
Illustration - Awwalu Sakiwa, Idowu Abayomi Oluwasegun
Language - Kiswahili
Level - Longer paragraphs