Siku moja, Sungura alikuwa anatembea ukingoni mwa mto.
Kiboko alikuwa akila majani matamu ya kijani.
Kwa bahati mbaya, Kiboko alimkanyaga Sungura mguuni.
Kwa uchungu, Sungura alipiga mayowe na kumfokea Kiboko akisema, "Wewe Kiboko! Unaukanyaga mguu wangu. Huoni?"
Kiboko alimuomba Sungura msamaha, "Samahani sana rafiki. Sikukusudia. Naomba unisamehe!"
Sungura hakumsikiliza. Aliendelea kumfokea Kiboko akisema, "Umefanya makusudi! Siku moja nitalipiza kisasi!"
Siku moja, Sungura alimtafuta Moto na kumwambia, "Naomba umuunguze Kiboko atakapotoka kwenye maji baada ya kula majani. Kanikanyaga!"
Moto akajibu, "Hapana shaka, rafiki yangu Sungura. Nitafanya ulivyoniambia."
Kiboko alipokuwa akila majani kando ya mto, "Whuuush!" Moto akalipuka na kuanza kuyaunguza manyoya ya Kiboko.
Kiboko alilia kwa uchungu huku akikimbilia majini. Manyoya yake yote yaliungua.
Kiboko alipiga mayowe, "Manyoya yangu yameunguzwa! Moto ameyaunguza manyoya yangu yote! Manyoya yangu yameungua! Manyoya yangu mazuri!"
Tangu wakati huo, kiboko hatembei mbali na maji kwa kuhofia kuunguzwa na Moto.
Sungura alifurahi sana kumuona Kiboko bila manyoya. Akasema, "Nimelipiza kisasi!"