Hadithi kumhusu Wangari Maathai
Nicola Rijsdijk
Maya Marshak

Kulikuwa na msichana mdogo aliyefanya kazi shambani na mamake.

Waliishi karibu na Mlima Kenya, Afrika Mashariki.

Msichana huyo aliitwa Wangari.

1

Wangari alilima katika bustani ya familia yake.

Alipanda mbegu ndogo katika ardhi iliyokuwa na joto.

2

Alipenda majira ya jioni, wakati jua lilipotua.

Giza lilipozidi, Wangari alirudi nyumbani.

3

Wangari alikuwa mwerevu. Alikuwa na hamu ya kwenda shule lakini, wazazi wake walitaka awasaidie nyumbani.

Alipofikisha umri wa miaka saba, alikubaliwa akaanza kwenda shule.

4

Wangari alipenda kusoma na kujifunza kupitia kila kitabu alichosoma. Alifanya vyema akaalikwa kwenda Amerika kuendeleza masoma yake.

Alichangamshwa sana na nafasi hii. Alipenda kuufahamu ulimwengu zaidi.

5

Alipokuwa chuoni huko Amerika, Wangari alijifunza mambo mapya. Alisomea mimea na jinsi inavyokua.

Alikumbuka vile alivyocheza na ndugu zake. Vilevile, alikumbuka kivuli cha miti maridadi ya misitu ya Kenya.

6

Alipojifunza, alifahamu kuwa aliwapenda watu wa Kenya. Alitaka wafurahi na wawe huru.

Alikumbuka kwao nyumbani Afrika.

7

Wangari alikamilisha masomo yake akarudi Kenya. Nchi yake ilikuwa imebadilika sana.

Watu matajiri walikuwa wameikata miti. Wanawake walikosa kuni.

Watu wengi walikuwa maskini. Watoto walikuwa na njaa.

8

Wangari aliwafunza wanawake kupanda miti. Waliiuza miti hiyo na kupata pesa.

Walizitumia kwa mahitaji ya familia zao. Walifurahi kwa sababu Wangari aliwasaidia kuwa na nguvu na uwezo.

9

Muda ulipopita, miti mipya ilikuwa misitu. Mito ilianza tena kupitisha maji.

Ujumbe wa Wangari ulienea Afrika nzima.

Leo, mamilioni ya miti imesitawi kutokana na juhudi za Wangari.

10

Watu ulimwengu mzima walifahamu bidii ambayo Wangari alikuwa amefanya.

Walimpa Tuzo la Amani la Nobel.

Wangari alikuwa mwanamke wa kwanza wa Kiafrika kupokea tuzo hilo.

11

Wangari aliaga dunia mwaka 2011.

Tunaweza kumfikiria kila tunapouona mti wa kupendeza.

12
You are free to download, copy, translate or adapt this story and use the illustrations as long as you attribute in the following way:
Hadithi kumhusu Wangari Maathai
Author - Nicola Rijsdijk
Translation - Ursula Nafula
Illustration - Maya Marshak
Language - Kiswahili
Level - First paragraphs