Mbuzi, Mbwa na Ng'ombe walikuwa marafiki wakubwa. Siku moja walisafiri kwa teksi.
Walifika mwisho wa safari yao. Dereva aliwauliza walipe nauli zao. Ng'ombe akalipa.
Mbwa hakuwa na kiasi kamili cha pesa, akalipa zaidi kidogo.
Dereva alikuwa anajitayarisha kumrudhishia Mbwa baki ya pesa zake. Wakati huo, Mbuzi alitoroka bila kulipa chochote.
Dereva akakasirika sana. Akaondosha gari bila kumrudishia Mbwa baki ya pesa zake.
Hiyo ndiyo sababu, siku zote, Mbwa hulikimbilia gari. Nia yake ni kumpata dereva amrudishie baki ya pesa zake.
Mbuzi, anapousikia mlio wa gari, hutoroka. Yeye huogopa kushikwa kwa kukosa kulipa nauli.
Ng'ombe huwa hashughuliki gari linapokuja. Yeye huchukua muda kuvuka barabara. Anajua kwamba alilipa nauli yake kamili!